20 Percent awekwa lock-up Zanzibar

 

Msanii wa Bongo Flava mwenye matatizo mengi 20 Percent amejikuta mikononi mwa polisi kwa mara nyingine tena lakini awamu hii ni visiwani Zanzibar.

Chanzo cha yote hayo ni kukataa kupanda na kuperform kwenye tuzo za muziki za Zanzibar.

Akiongea na Clouds Fm leo, Afande Sele ambaye naye alikuwa miongoni mwa wasanii walioalikwa kwenye tuzo hizo amesema waandaji wa tuzo hizo waliingia makubaliano na 20 Percent kuwa watamlipa shilingi milioni moja lakini atajigharamikia vitu vingine.

Afande amesema hata hivyo mpaka anaondoka Morogoro, 20 Percent alikuwa hajajiandaa na hivyo alienda akiwa amechelewa.

Ugomvi ulianza baada ya 20 kufika Zanzibar ambapo alitaka aongezewe hela zingine wakati mkataba ulisema alitakiwa kulipwa shilingi milioni moja peke yake.

Kufuatia hali hiyo 20 alikataa kuperform na ndipo Afande aliokoa jahazi na kuondoa aibu kwa kuimba nyimbo mbili.

Waandaaji hao waliamua kumpeleka polisi kwenye kituo cha Madema visiwani humo ambapo walishikilia vitu vyake ikiwa ni pamoja na laptop.

Hata hivyo 20 ameshatoka na anatakiwa kuwalipa shilingi milioni moja yao ili wamrudishie vitu vyake.

Afande ameelezea kusikitishwa kwake kutokana na kitendo alichokifanya swahiba wake.